Rais wa Shirikisho la Soka Barani Ulaya ‘UEFA’ Aleksander Ceferin, amesema kashfa ya waamuzi inayoikabili FC Barcelona ni moja ya hali mbaya zaidi ambayo amewahi kuona katika soka.

Mwezi Machi mwaka huu, Shirikisho la Soka Barani Ulaya lilifungua uchunguzi kuhusu malipo ambayo Barca ilitoa kwa makamu wa Rais wa zamani wa kamati ya waamuzi ya Hispania.

Kuanzia mwaka 2001 hadi 2018, Barca ililipa zaidi ya Euro Milioni saba kwa Jose Maria Enriquez Negreira.

Klabu hiyo ya Katalunya imesema walikuwa wakinunua ripoti za kiufundi kuhusu waamuzi na wanakana kuwahi kununua maafisa wa mechi au ushawishi.

“Hali ni mbaya sana,” alisema Ceferin katika mahojiano na gazeti la nchini Slovenia, Ekipa, alipoulizwa kuhusu matukio yanayoizunguka Barca.

“Ni mbaya sana, kwa maoni yangu ni moja ya hali mbaya zaidi katika soka ambayo nimewahi kuona,” amesema.

Waendesha mashtaka wanafuatilia mashtaka dhidi ya Barca kwa madai ya rushwa, huku mahakama nchini Hispania ikikubali kufungua uchunguzi kuhusu klabu hiyo na marais wa zamani, Sandro Rosell na Josep Maria Bartomeu.

Real Madrid na mashirika kadhaa ya michezo nchini humo pia yamejiunga na kesi ya waendesha mashtaka.

Rais wa LaLiga, Javier Tebas ameitaja kashfa hiyo kuwa mgogoro mbaya zaidi wa sifa anaoweza kuukumbuka katika soka la Hispania na kumtaka Rais wa Barca, Joan Laporta kufuta malipo hayo.

Laporta alisema anapanga kufanya mkutano na wanahabari mara tu uchunguzi wa ndani utakapokamilika.

Lakini Tebas pia amethibitisha La Liga haitaweza kuiadhibu Barca kwa sababu ya sheria ya mapungufu ya nchini Hispania ingawa Ceferin alifichua UEFA haikabiliwi na vikwazo kama hivyo.

“Siwezi kutoa maoni moja kwa moja juu ya hili kwa sababu mbili,” amesema Ceferin.

“Kwanza kwa sababu tuna kamati huru ya nidhamu inayosimamia hili, na pili, kwa sababu sijashughulikia suala hili kwa undani.” “Katika kiwango cha LaLiga, bila shaka, suala hilo limezuiliwa kwa muda na haliwezi kuwa na matokeo ya ushindani, lakini kesi zinaendelea katika ngazi ya waendesha mashtaka. Lakini kuhusu UEFA, hakuna kitu kilichozuiliwa na muda.”

Wajumbe 555 usimamizi maafa wapata mafunzo kuimarisha uwezo
Fiston Mayele aitamani Simba SC April 16