Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky, ametoa tena wito wa kufanya mkutano na kiongozi wa Urusi Vladimir Putin, katika juhudi za kumaliza vita nchini mwake.
Katika mkutano na waandishi wa habari Zelensky amesema hakuwa na hofu ya kukutana na Putin iwapo hilo lingesababisha makubaliano ya amani kati ya mataifa hayo mawili.
Ameongeza kuwa tangu mwanzo amekuwa akisisitiza mazungumzo na rais Putin.
Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Antony Blinken atazuru Kyiv leo Jumapili, siku ambayo uvamizi wa Urusi dhidi ya Ukraine unaingia mwezi wake wa tatu.
Afisa wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani amekataa kuzungumzia ziara hiyo ya kwanza rasmi ya maafisa wa serikali.
Rais Zelenskiy ameishutumu mipango ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres kutembelea Moscow siku ya Jumanne, kabla ya Kyiv, akisema hakuna haki wala mantiki katika utaratibu huo.
Zelensky amerudia onyo lake kwamba watavunja mazungumzo ikiwa Urusi itawaua wanajeshi wa Ukraine waliosalia katika bandari iliyozingirwa ya Bahari Nyeusi ya Mariupol.