Rais wa Ufilipino, Rodrigo Duterte leo amevitaka vikosi vya Marekani vilivyoko nchini humo kuondoka mara moja akidai kuwa wanaweza kumleta balaa la kushambuliwa na magaidi wa ISIS.

Kauli hiyo ya Duterte imekuja ikiwa ni wiki moja tangu amulikwe na vyombo vya habari kwa kumtolea tusi Rais wa Marekani, Barack Obama hali iliyopelekea Rais huyo wa Marekani kuahirisha mkutano kati ya wawili hao.

Akihutubia taifa hilo baada ya kuapishwa, Duterte alisema kuwa vikosi maalum vya Marekani vinavyoendesha mafunzo kwa Jeshi la Ufilipino havina budi kuondoka kwani vinavutia kundi la Abu Sayyaf lenye uhusiano na ISIS kufanya mashambulizi nchini humo vikilenga kuwakamata na kuwachinja wanajeshi wa Marekani.

“Hivi vikosi vya Marekani lazima viondoke. [Abu Sayyaf] itawatafuta na kuwaua, itawateka kwa malengo ya kujipatia fedha au wafungwa wao kwa kubadilishana nao,” alisema Duterte.

Kauli za rais huyo zimeanza kuonekana kama tishio la uhusiano kati ya Ufilipino na Marekani ambayo iliwahi kutawala taifa hilo la bara la Asia.

Waiba Mashine za kupima tetemeko la ardhi
Viongozi wa dini watakiwa kutumia nyumba za ibada kuhamasisha amani