Mlinda Lango Ramadhan Kabwili amewaaga Mashabiki na Wanachama wa Klabu ya Young Africans, baada ya kumaliza mkataba wake na klabu hiyo, iliyotwaa Ubingwa wa Tanzania Bara msimu huu 2021/22.
Kabwili ambaye alikua sehemu ya kikosi cha Young Africans licha ya kutocheza ama kufanya mazoezi na kikosi cha klabu hiyo kwa msimu huu, ametoa neno la shukurani kupitia kurasa zake za Mitandao ya Kijamii.
Ameandika maneno mazito wa shukurani na kuahidi kuendelea kuithamini na kuikumbuka Young Africans, ambayo ameitumikia kwa miaka mitano kwa mujibu wa mkataba wake, ambao umefikia tamati.
Kabwili ameandika: “Nipende kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa muda wote wa miaka 5 niliotumikia Yanga nasema ahsante na Mungu awabariki mtabaki kichwani mwangu daima.”
“Nimejifunza mengi hasa kuamini kila nyakati za misimu bila kukata tamaa katika kazi yangu na mme nisaidia kunikomaza kwa hali zote za maisha yangu leo najivunia kwa Watanzania mashabiki, viongozi na wachezaji wenzangu mtabakia milele kichwani mwangu Asante wananchi,”
Kabwili aliwahi kuwa sehemu ya kikosi cha kwanza cha Young Africans wakati wa Kocha Mwinyi Zahera, huku akitumikia udhaifu wa Mlinda Lango kutoka DR Congo aliyekua chaguo la kwanza kipindi hicho Claus Kindoki.