Beki wa kati kutoka Ufaransa na Klabu ya Manchester United, Raphael Varane amesema Erik ten Hag ameonesha kuwa hana hofu ya kufanya maamuzi makubwa baada ya kocha huyo kumchagua kiungo Bruno Fernandez kuwa nahodha mpya wa klabu hiyo.
Awali nafasi hiyo ilikuwa ikishikiliwa na Harry Maguire ambaye amekuwa nahodha wa Manchester United tangu alipojiunga nao akitokea Leicester mwaka 2019.
Ni uamuzi mkubwa aliofanya kocha huyo kwa siku za baada ya ule wa kuwaweka benchi Cristiano Ronaldo na Marcus Rashford kwa utovu wa nidhamu msimu uliopita.
Varane alisema kufanya mabadiliko ya nahodha inaonesha kuwa Ten Hag yuko mstari wa mbele kuiongoza timu hiyo.
“Anataka timu yenye kupambana na yeye ni kiongozi hivyo anatakiwa kuonesha kwa vitendo,” alisema Varane alipozungumza na ESPN.
“Hana hofu ya kufanya maamuzi kama haya na kuwajibika. Hicho ndicho tunachotarajia kutoka kwa kocha. Amefanya hivyo hivyo nadhani, kwenye mambo kama haya unaongoza kwa mfano.
“Anajua nini hasa anataka. Ameonesha hiyo dhamira na katika siku yake ya kwanza tulijua nini tunatakiwa kufanya na wapi anataka kuelekea. Yote yako wazi kwa wachezaji na timu na tuna mahusiano mazuri na kocha.”
Manchester United kwa sasa wako Marekani wakijiwinda na msimu ujao wa Ligi Kuu ya England na michuano mingine ya kimataifa.