Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Dkt. Kebwe Stephen Kebwe ameviagiza vyombo vya Ulinzi na Usalama vya Mkoa na Wilaya ya Kilosa kuwakamata wale wote wanaotuhumiwa kuwavamia wananchi wanaolima katika mashamba yaliyofutiwa umiliki wake na Rais John Pombe Magufuli.

Ametoa agizo alipofanya ziara Wilayani Kilosa iliyolenga kujiridhisha utekelezaji wa mashamba yaliyofutwa mwaka 2017 na Rais wa Jamhuri ya Muuungano wa Tanzania na kuagiza mashamba hayo kupangiwa matumizi mengine ikiwa ni pamoja na kuyagawa kwa wananchi wa maeneo jirani na mashamba hayo.

Aidha, Mkuu huyo wa Mkoa amewahakikishia wananchi wa vijiji hivyo kuwa kila mtu ambaye hana eneo la kulima atapatiwa kupitia mashamba hayo yaliyofutwa na Rais ili kila mwananchi aweze kuzalisha na kujikimu kimaisha huku akionya kutoingiza itikadi ya aina yoyote kwenye mashamba hayo yaliyofutwa na Rais.

“Vyombo vyangu vinaniambia wale walikwenda wakavamia maeneo hayo walitaka waanzishe mpango mwingine mpya, yaani juhudi zote hizi ambazo Serikali imefanya kwake yeye si kitu. sasa hao mtusaidie tuwafahamu ni akina nani na tuwachukulie hatua, sio kuwafahamu tu,”amesema Dkt. Kebwe.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Kilosa, Adam Mgoyi amewataka wananchi wa vijiji vya Mvumi na Gongwe kukomesha tabia ya ubishi na ugomvi baina yao, badala yake watekeleze maagizo ya Serikali yaliyotolewa na Mkuu wa Mkoa na kuwatahadhalisha kuwa atakayekwenda kinyume na maagizo hayo atakamatwa na kuchukuliwa hatua za sheria.

Kwa mujibu wa Afisa Ardhi Wilaya ya Kilosa, Ibrahim Ndembo amesema kuwa Mashamba hayo matano Na. 32 hadi 36 yenye jumla ya Ekari 2,685, baada ya Rais kuyafuta, Wilaya ilipeleka maombi Serikalini ili kupewa idhini ya kutumia mashamba hayo kwa muda ombi ambalo lilikubaliwa.

 

Tume ya Uchaguzi NEC yaanza maandalizi ya uchaguzi mkuu 2020
JPM atoa neno kuhusu tukio la kutekwa kwa Mo Dewji