Mkuu wa Mkoa wa Pwani ,Aboubakar Kunenge ametoa onyo kwa watu wanaojihusisha na uhalifu wa aina mbalimbali ikiwemo wizi, ubakaji, kuvamia nyumba za ibada, matumizi ya dawa ya kulevya na uingizaji wahamiaji haramu, kuacha mara moja.
Amesema kuwa endapo watakaidi agizo hilo na kuendelea na uhalifu wa aina yoyote ile kitakachofuata ni kuchukuliwa hatua stahiki za kisheria dhidi yao.
Akizungumza mjini Kibaha na viongozi wa madhehebu mbalimbali mkoani Pwani Kunenge amesema kuwa, wameshatoa matamko mengi kwa wananchi lakini baadhi ya watu bado wanaendelea kujihusisha na matukio hayo ambayo ni kero kwa wananchi.
“Serikali imekuwa ikijitahidi kutoa elimu na ushauri kwa wananchi kutojihusisha na vitendo vya uhalifu lakini bado wanaendeleza vitendo vya kihalifu,” Amsema RC Kunenge.
Aidha ameendelea kuwahimiza viongozi wa kidini kushirikiana na serikali kuwatangazia waumini wao juu ya kuacha vitendo hivyo viovu au kushirikiana na wahalifu.
Naye mwenyekiti mwenza wa kamati ya amani ya Mkoa, Beno Kikudo amesema baadhi ya watu wanakiuka maadili ya imani zao na kusababisha vitendo viovu kuendelea ndani ya jamii.