Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Aboubakar Kunenge amepiga marufuku baadhi ya masoko kupangisha vizimba kwa madalali kisha madalali hao kuwapangishia wananchi kwa bei ya juu.
Amesema hayo wakati akitembelea mradi wa soko la Tandale ambapo amemtaka mkandarasi kukamilisha mradi huo ifikapo mwezi wa nne mwakani kutokana na umuhimu mkubwa wa soko hilo.
Aidha amemtaka mkandarasi wa kamapuni ya Mecco inayojenga soko la kibada kuhakikisha anakamilisha ujenzi kabla ya mwezi wa tano ili wananchi waweze kunufaika na Manispaa ipate mapato.
Hatahivyo, Kunenge amesema jambo la kuwapangisha vibanda kwa bei kubwa linawaumiza wafanyabiashara wadogo wakati lengo la Serikali kujenga masoko hayo, ilikuwa ni kuwasaidia wafanyabiashara na sio kuwakandamiza.
RC Kunenge amesema masoko yanayojengwa yakikamilika na wafanyabiashara wakapangiwa sehemu za kuuza, bidhaa zao ni marufuku kwa mfanyabiashara kufanya biashara nje ya masoko au sehemu zisizo rasmi.