Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Mhe. Amos Makalla amesema Mkoa huo umedhamiria kuanzisha One stop center ya biashara kwa lengo la Kuweka mazingira wezeshi ya Biashara na Uwekezaji na kuondoa urasimu na rushwa ambayo inatarajiwa kuwa tayari Septemba mosi mwaka huu.
RC Makalla amesema One stop center hiyo itajumuisha Taasisi zote husika ikiwemo TRA, BRELA, OSHA, NEMC, Fire na Wadau wote wa Biashara ambapo itasaidia pia kuondoa ucheleweshaji wa kupata vibali, leseni, usumbufu na Mwingiliano wa majukumu ya kitaasisi.
Akizungumza wakati wa Barazaa la Biashara Dar es salaam RC Makalla amewahakikishia Wafanyabiashara usalama wa Biashara zao na kuwataka kutoa taarifa kwa Jeshi la Polisi wakiona Viashiria vya uhalifu.
Aidha RC Makalla ametoa wito kwa Mamlaka zinazohusika na ukusanyaji wa Mapato kuhakikisha wanakusanya Kodi kwa mujibu wa Sheria pasipo uonevu Wala usumbufu kwa Wafanyabiashara.
Pamoja na hayo RC Makalla ameipongeza Bank ya NMB kwa uamuzi wa kulipa kiasi Cha Shilingi Milioni 438 kama bima kwa Wafanyabiashara Soko la Kariakoo waliounguliwa Mali zao.
Hata hivyo RC Makalla ameagiza Watendaji wa Mkoa huo kuhakikisha wanakuwa Mstari wa mbele Katika kupatia ufumbuzi kero na changamoto za Wafanyabiashara ili kuondoa Manung’uniko.