Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Amos Makalla amewataka majambazi na wahalifu kujisalimisha polisi na kukabidhi silaha zao huku akitangaza operesheni ya kuwasaka popote walipo.
Ametoa kauli hiyo leo Jumanne Mei 25, 2021 baada ya kikao chake na makamanda wa polisi huku akirejea matukio yaliyotokea hivi karibuni likiwemo la Mbezi ambapo Jimmy Kibiti aliuawa kwa kupigwa risasi wakati akitoka benki na kuporwa Sh Milioni 4 na la jana la mfanyabiashara kujeruhiwa kwa risasi eneo la Mabibo.
“Nataka Dar es Salaam iwe mahali salama. Tunawaonya waache mara moja, matukio hayo mawili waliyoyafanya yanatosha. Hawa wanabip sisi tuna bando la kutosha. Tunawaonyesha shoo kwa shoo kwamba polisi wapo, watakuwa fundisho kwa wengine,” amesema RC Makalla.
“Wasijaribu njiti kama zimejaa kwa kutingisha kiberiti. Niseme tu wasalimishe silaha, kamanda Wambura (Camillius) sikufundishi kazi ila nakwambia wanyang’anye, najua wapo watakaotoa kwa hiari na wale mtakaowakuta nazo wanyang’anyeni,” ameonya RC Makalla.
Katika mkutano na wanahabari, Wambura ametoa onyo kwa wahalifu akiwataka kuacha mara moja, “wasijaribu kupima kina cha maji kwa miguu yao kwani ni mifupi. Tunawaonya wale wote wanaotaka kucheza na jeshi la polisi, wajitathmini kwanza. Wale wote wanaotaka kushindana na Serikali wakae chonjo saa mbaya, wasijaribu kupima kina cha maji na miguu yao mifupi, wajitathmini kwanza.”
Aidha, alieleza kuwa polisi wamekamata bunduki aina ya Short Gun Pump, watuhumiwa 20, magari manne pamoja na pikipiki moja.