Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam, Paul Makonda amesema kuwa atawasilisha muswada wa mapendekezo ya mabadiliko ya Sheria ya mirathi na sheria ya Ndoa kwa Waziri wa Katiba na Sheria ili ziweze kufanyiwa marekebisho kutokana na sheria hizo kupitwa na wakati.
Makonda amesema kuwa sheria hizo zimeonekana kuwa kandamizi kwa wanawake wengi zaidi, hasa kile kipindi mwanaume anapofariki, jambo linalopelekea mateso na manyanyaso kwa wajane.
“Sheria kandamizi zinazotakiwa kufanyiwa mabadiliko ni sheria ya Kiserikali ya mirathi, sheria ya mirathi ya kimila ya Mwaka 1963 na Sheria ya Mirathi ya kidini ya Mwaka 1963,”amesema Makonda.
Aidha, Makonda ameshauri mara baada ya sheria kufanyiwa maboresho iweze kumpa uhalali Mke wa marehemu kushiriki katika vikao vya mgawanyo wa mali, pamoja na usawa wa watoto katika kumiliki mali za marehemu bila kujali jinsia pamoja na haki ya mtoto wa nje ya ndoa kurithi Mali.