Ripoti ya kushtua iliyotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) imebainisha kiwango kikubwa cha watanzania wanaolirudisha nyuma taifa kimaendeleo kwa kutofanya kazi huku wakitumia muda mwingi kulala, kupiga zogo, kufanya starehe na kufanya shughuli zisizowaingizia kipato.

Kwa mujibu wa Ripoti hiyo ya utafiti wa watu wenye uwezo wa kufanya kazi nchini iliyozinduliwa na Waziri wa Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Ajira na watu wenye Ulemavu, Jenista Mhagama, inaonesha kuwa watu hutumia 71% ya saa za kazi katika kufanya shughuli zisizozalisha ikiwa ni pamoja na kujihusisha na starehe.

Akifafanua kuhusu ripoti hiyo, Mkurugenzi wa NBS, Dk. Albina Chuwa alisema kuwa asilimia 16.5 ya wanawake hutumia muda mwingi katika kufanya kazi za nyumbani zisizowaingizia kipato, huku asilimia 4.4 ya wanaume wakiwa katika kundi hilo pia.

Aidha, Waziri Mhagama alieleza kuwa Serikali ya Awamu ya Tano tayari ilishaliona tatizo hilo na ndio sababu ikaja na sera ya ‘Hapa Kazi Tu’.

“Ina maanisha 29% ya muda, ndio watanzania wanaotumia kufanya kazi. Hii ni aibu kubwa na haiwezi kuvumiliwa wala kufumbiwa macho hata kidogo,” alisema Mhagama.

Aliongeza kuwa nchi haiwezi kuendelea bila watu wake kufanya kazi kwani njia pekee ya kuondoa umasikini ni kufanya kazi.

Ripoti hiyo imeonesha kuwa watanzania wenye uwezo wa kufanya kazi ni milioni 22.3 na kati ya hao milioni 2.3 hawafanyi kazi.

Mashabiki 15,000 Kushuhudia Game Ya Al Ahly Vs Young Africans
Aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Tanesco apenya mahakamani