Mashabiki wasiozidi 15,000 watapewa nafasi ya kushudia mchezo wa mkondo wa pili wa ligi ya mabingwa barani Afrika, kati ya Al Ahly ya Misri na Young Afrika ya Tanzania utakaochezwa kwenye uwanja wa Alexandria, uliopo katika kitongoji cha Borg Al-Arab mjini Alexandria.

Taarifa kutoka chama cha soka nchini Misri zimeeleza kwamba, licha ya uwanja huo kuwa na uwezo wa kuchukua mashabiki 86,000, wameona kuna umuhimu wa mashabiki wachache kupatiwa nafasi hiyo kwa kuhofia hali ya kiusalama.

Mkurugenzi mtendaji wa Chama cha Kandanda cha Misri (EFA), Tharwat Swilan amethibitisha tiketi hizo 15,000 za kuingilia uwanjani kwa ajili ya mchezo huo hazitauzwa kwa mashabiki kwa njia ya kawaida.

Amesema mashabiki watajaza fomu za maombi ya tiketi mtandaoni kisha bahati nasibu kuchezeshwa kwa ajili ya kuchagua mashabiki watakaotumiwa mualiko wa kuingia uwanjani.

Kikosi cha Young Africans kitakua mgeni wa Al Ahly katika mchezo wa mkondo wa pili utakaochezwa siku ya Jumatano.

Wawakilishi hao wa Tanzania wanahitaji ushindi wa aina yoyote au sare ya kuanzia mabao 2 ili kuweza kutinga katika hatua ya makundi kwa mara ya pili kwenye historia yao.

Shomari Kapombe Arejea Nyumbani Tanzania
Ripoti: Watanzania wengi hawataki kazi, hutumia muda mwingi kulala, starehe