Beki kisiki wa Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, Shomari Kapombe, amerejea nchini baada ya wataalamu wa Hospitali ya Morningside Mediclinic ya jijini Johannesburg, Afrika Kusini kurishidhwa na maendeleo ya afya yake.

Kapombe alikuwa jijini humo katika hospitali hiyo tokea Alhamisi iliyopita akipatiwa matibabu baada ya kugundulika anasumbuliwa na ugonjwa wa Pulmonary Embolism (donge la damu kuziba mishipa ya damu katika mapafu) na sasa afya yake imezidi kuimarika hali iliyopelekea kuruhusiwa kutoka hospitali.

Daktari Mkuu wa Azam FC, Dr. Juma Mwimbe, ameuthibitshia mtandao wa klabu www.azamfc.co.tz kuhusu kurejea kwa Kapombe na amedai kuwa kwa sasa yupo kwenye mapumziko nyumbani kwake akiendelea na dozi ya matibabu aliyopewa na wataalamu hao kutoka Afrika Kusini.

Kwa mujibu wa Mwimbe ameweka wazi kuwa Kapombe atakosekana uwanjani kwa kipindi chote kilichobakia cha msimu huu na huenda akarejea uwanjani wakati Azam FC itakapoanza kujiandaa na msimu ujao, lakini bado atakuwa akiendela na dozi aliyopewa kwani itamchukua si chini ya mwaka mmoja hadi miwili hadi kuweza kumaliza matibabu yote.

“Hiyo haimaanishi atakuwa hachezi bali kutokana na madhara aliyopata na aina ya ugonjwa kitaalamu atahitaji kutumia dozi ya aina hiyo kwa muda usiopungua mwaka mmoja au miwili ili mwili wake mzima urejee kwenye hali ya kawaida, lakini mara baada ya mapumziko ya miezi miwili hadi mitatu anayotakiwa kupumzika ataruhusiwa kucheza huku akiendelea na dozi,” alisema.

Beki huyo wa zamani wa Simba na AS Cannes ya Ufaransa, amekuwa na kiwango kizuri msimu huu kwani mpaka sasa ameshaifungia Azam FC mabao 11, nane kwenye Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL), mawili Kombe la Shirikisho (Azam Sports Federation Cup) na moja amepachika ndani ya Kombe la Shirikisho Afrika (CC) wakati timu hiyo ikiilaza Bidvest Wits mabao 3-0.

Anne Kilango afananisha yaliyomsibu na ‘Msiba’
Mashabiki 15,000 Kushuhudia Game Ya Al Ahly Vs Young Africans