Kocha Mkuu wa Simba SC Roberti Oliveira ‘Robertinho’ amefichua siri ya ushindi dhidi ya Mabingwa wa Soka nchini Uganda Vipers SC, katika mchezo wa Mzunguuko watatu wa Kundi C, Ligi ya Mabingwa Barani Afrika.
Vipers SC ilikuwa nyumbani katika Uwanja wa St Mary’s-Kitende mjini Entebe, ikiikaribisha Simba SC kutoka Tanzania juzi Jumamosi (Februari 25).
Kocha Robertonho amefichua siri ya ushindi wa 0-1, baada ya kuwasili jijini Dar es salaam jana Jumapili (Februari 26), tayari kwa maandalizi ya mchezo wa Mzunguuko wanne utakaopigwa Jumamosi (Machi 04), Uwanja wa Benjamin Mkapa.
Robertino amesema kitendo cha kuifahamu vizuri Vipers SC kilimsaidia kupanga mfumo wa tofauti, ambao uliwanyima Mabeki wa timu hiyo ya Uganda kutambua nani alipaswa kukabwa kama Mshambuliaji wa Mwisho wa Simba SC.
Amesema Vipers SC aliyokuwa akiinoa kabla ya kutua Simba SC mwezi Januari-2023, ina wachezaji wazuri na wenye kasi kubwa, hivyo mfumo alioutumia ulivuruga mipango yao na kuwalazimisha kucheza kwa tahadhari kubwa.
“Vipers nawajua vizuri wanacheza mchezo wa kasi na kushtukiza, hivyo nihitaji kuingia na watu wenye nguvu ya kushambulia na kukaba kwa nguvu na haraka kama Kibu,”
“Kama ulivyoona kuna muda walishindwa kujua mshambuliaji wa mwisho ni nani ili wamkabe, kwani Phiri, Kibu na Saido walikuwa wanabadilishana maeneo na hilo lilitusaidia kuwafanya mabeki wa Vipers kutopanda juu na muda mwingi kubaki kwenye eneo lao,”
“Baada ya kupata bao tulihitaji kulilinda kwanza huku tukifanya mipango ya kutafuta mengine zaidi, na kadri muda ulivyozidi kwenda ilibidi tuongeze nguvu kwa kumwingiza Nyoni ili atulize presha na tukafanikiwa.” amesema Robertinho
Ushindi wa 0-1 umefufua matumaini ya Simba SC kutinga Robo Fainali Ligi ya Mabingwa Barani Afrika msimu huu, ikifisha alama tatu, huku ikikabiliwa na michezo miwili mfululizo nyumbani Dar es salaam dhidi ya Vipers SC na Horoya AC ya Guinea.
Raja Casablanca bado inaongoza msimamo wa Kundi C ikifikisha alama 09, ikifuatiwa na Horoya AC yenye alama 04, Simba SC inashika nafasi ya tatu kwa kuwa na alama 03, huku Vipers SC ikiburuza mkia kwa kuwa na alama 01.