Hatimaye Kocha Mkuu wa Simba SC Roberto Oliveira ‘Robertinho’, amafichua siri ya kuibanjua Young Africans katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, uliopigwa Juzi Jumapili (April 16), katika Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam.
Kocha huyo kutoka nchini Brazil amesema walichofanya wachezaji wa kikosi chake kwenye mchezo huo akiwemo Kibu Denis, ni maelekezo waliyoyafanyia kazi katika uwanja wa mazoezi siku kadhaa kabla ya mpambam huo.
Kocha Robertinho amesema walikuwa na muda mzuri kufanya maandalizi kwa ajili ya mchezo wao dhidi ya Young Africans jambo ambalo limewapa matokeo mazuri.
“Ilikuwa kazi kubwa kwa kila mmoja kutafuta ushindi, ambayo tuliifanya na imeonekana uwanjani, wachezaji wote Kibu Denis, Clatous Chama, Henock Inonga, Erasto Nyoni walifanya kazi kubwa.”
“Unapozungumzia Simba unaitaja timu kubwa na wapinzani wetu Young Africans nao sio timu ya kubeza kwani inafanya kazi kwa umakini, kikubwa ni kutafuta alama tatu ambazo tumezipata,” amesema Robertinho
Ushindi wa 2-0, umeiwezesha Simba SC kufikisha alama 63, ikiachwa kwa alama tano zaidi na Young Africans inayoendelea kuongoza msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara hadi sasa.