Wakati Kikosi cha Simba SC kikitarajia kuanza safari ya kuelekea Morocco leo Jumanne (Machi 28), Kocha Mkuu wa kikosi hicho Robertinho Oliveira ‘Robertinho’, ametuma salamu pongezi kwa wachezaji wake akisema kwa sasa wameanza kumwelewa aina ya soka ambalo yeye anataka wacheze.
Robertinho ambaye awali Wanachama, Mashabiki wa Simba SC na baadhi ya wachambuzi walionekana hawaelewi ni aina gani ya soka ambalo amelileta kwenye kikosi hicho, wakidai halivutil tofauti na zamani, amesema ana furaha sasa kwani kwenye michezo mitatu, miwili ya Ligi ya Mabingwa na mmoja ya Ligi Kuu dhidi ya Mtibwa Sugar, timu yake ilicheza kwa ufasaha aina ya soka ambalo ameingiza falsafa zake ndani ya kikosi.
“Angalia kwa sasa naweza kuwatumia Shomari Kapombe na Mohamed [Hussein ‘Tshabalala’] muda wote wanakwenda mbele kusaidia mashambulizi kwa kupiga krosi kushoto na kulia, kama mshambuliaji anakaa kwenye eneo sahihi anafunga bao kwa urahisi zaidi na hilo ndilo ninalohitaji,” alisema kocha huyo.”
Ameongeza kuwa kwenye mfumo wake kwa sasa ametoka kwenye kutumia Mshambuliaji mmoja na kuweka wawili ili wawe wanafanya kazi ya kumalizia krosi zinazopigwa pande zote kutoka kwa mabeki wake.
“Natumia Washambuliaji wawili ambao wanasubiri krosi wafunge kwa kichwa au mguu, nina furaha kwa sababu michezo mitatu iliyopita, timu yangu ilicheza vema sana, wachezaji wangu wamefunga mabao mengi, hatua kwa hatua tunabadilisha mtazamo kwa sababu baada ya kufanya shambulizi zuri, unatakiwa kumalizia kwa kupiga shuti.”
“Ni muhimu sana kupiga mashuti na kufunga, hiyo ni muhimu kwangu na kwa timu kwa jumla kwa sababu mwisho wa siku tunahitaji ushindi,” amesema kocha huyo kutoka Brazil
Kocha huyo alikuwa akilaumiwa kutokana na wachezaji wake kutocheza soka la kuvutia lililozoeleka kwa Simba ambalo ni la pasi za taratibu na kwenda mbele kwa pasi fupi fupi hadi langoni mwa wapinzani, lakini kwa sasa amelibadilisha na kuwa la kasi, wakishambulia kwa haraka mbele na kurejea haraka kukaba.