Mkuu wa Benchi la Ufundi Simba SC Roberto Oliviera ameitaka kamati ya usajili ya klabu hiyo kusajili wachezaji wanaolingana kiuwezo ili kupata uwiano sahihi pindi mmoja anapokosekana.
Kamati ya usajili pamoja na Mkuu wa Skauti Mels Daalder, tayari wameingia msituni kwa ajili ya kusaka nyota wapya ili kuboresha kikosi cha msimu ujao wa mashindano ikiwamo michuano ya ‘ CAF Super League’ inayotarajiwa kuanza Agosti mwaka huu.
Robertinho amesema anahitaji kuimarisha kikosi chake katika usajili kwa kila nafasi kuwe na wachezaji wawili au zaidi wenye ubora na kiwango kizuri.
“Msimu huu tumeshindwa kufikia malengo kwa sababu ya kukosekana kwa nyota wa kikosi cha kwanza kuumia na kushindwa kupata mbadala wao wenye uwiano mzuri na yule tuliyemkosa, tayari nimewasilisha ripoti na mapendekezo yangu, sasa ni muda wa kuandaa timu nzuri na imara kuhakikisha tunafanya usajili mkubwa kulingana na malengo yetu tuliyojiwekea,” amesema Robertinho
Ameongeza kuwa wanahitaji kubadilisha fikra za wachezaji na mipango yao kwa ajili ya msimu ujao ambao wamepania kurejesha makali yao.
Miongoni majina yaliyopendekezwa, ni Mlinda Lango wa Vipers FC ya Uganda, Alfred Mudekereza ambaye anatarajiwa kumpa changamoto Aishi Manula sambamba na Ally Salim, huku Beno Kakolanya akitarajia kuondoka mwishoni mwa msimu huu.
Kipa huyo namba moja wa Vipers United ameonyesha kiwango kizuri katika michuano ya kimataifa na kupendekezwa kuwa miongoni mwa nyota watakaosajiliwa kwa msimu ujao wa mashindano.
Chanzo cha ndani kutoka Simba SC kimesema kuwa Robertinho amewataka viongozi kuhusu suala la kipa walifanyie kazi mapema ili kuziba nafasi ya Beno Kakolanya.