Baada ya kufuzu kwa mbinde hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika, Kocha Mkuu wa Simba SC, Robertinho Oliveira, amesema kikubwa ni timu yake imevuka kucheza hatua hiyo kwani walikutana na mpinzani mgumu.
Amesema kwa kiasi kikubwa benchi la ufundi na wachezaji wamefurahi kuingia hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika na kujiandaa na yaliyopo mbele yao ili kufikia malengo.
Simba SC imefuzu hatua ya makundi baada ya kuitoa Power Dynamos kwa faida ya bao la ugenini kutokana na kutoka sare ya mabao 2-2 nchini Zambia kabla ya juzi Jumapili (Oktoba Mosi) kutoka tena sare ya bao 1-1 kwenye Uwanja wa Azam Complex, Dar es salaam.
Kocha Robertinho amesema lengo la kwanza lilikuwa kuhakikisha timu inaingia hatua ya makundi kwa kuitoa Power Dynamos na hilo limefanikiwa.
Amewapongeza wachezaji kwa kutokata tamaa hadi mwisho akidai Power Dynamos ni timu bora na ilikuwa imejipanga vizuri kwa michezo yote miwili ya nyumbani na ugenini.
Kuhusu kumwingiza John Bocco aliyesababisha kupatikana kwa bao la kusawazisha, Robertinho amesema: “Nilifanya mabadiliko hayo kipindi cha pili kwa kuwa niliwaona Dynamos wote wamerudi nyuma na waliziba mianya ya kupitisha pasi, alitakiwa mtu wa kusimama na mabeki wao na alienda kufanya kazi niliyomtuma.
“Baada ya Power Dyrnamos kupata bao, walirudi nyuma wote ikawa ngumu kupitisha mipira ikabidi tumwingize Bocco kwa kuwa ni mrefu angeweza kucheza sambamba nao tuliongeza kasi iliyosababisha kupatikana kwa bao la kusawazisha,” amesema kocha huyo.
Kiungo wa Simba SC, Said Ntibazonkiza, amesema mechi ilikuwa ngumu na walipambana kwa dakika zote na kufanikiwa kufuzu na kucheza hatua ya makundi.
Amesema mechi imeisha wanaangalla zaidi yaliyopo mbele kuendelea kupambania timu kufanya vizuri na kufikia malengo yanayotarajiwa na Wanasimbazi.
“Niwaombe tu mashabiki na wadau wa Simba SC kuwa na uvumilivu kwa kuwa siku zote hatutakuwa na mechi rahisi, kwa sababu tumecheza na timu ngumu sana, lakini wasikate tamaa na waendelee kutoa sapoti kwa benchi la ufundi kwenye mabadiliko anayoyafanya,” amesema.