Kocha Mkuu wa Simba SC Roberto Oliveira ‘Robertinho’ anatarajiwa kurejea jijini Dar es salaam leo Jumanne (Januari 31), akitokea nchini kwao Brazil.
Robertinho alirudi kwao Brazil baada ya mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya Dodoma Jiji FC uliomalizika kwa Simba SC kupata ushindi wa 1-0, mjini Dodoma.
Kocha huyo mwenye umri wa miaka 62, amesema anatarajia kuwasili Dar es salaam saa nne usiku, na kesho asubuhi atakuwa mazoezini.
“Nitafika hapo Dar es salaam leo usiku tayari kwa kuungana na timu, ili kuendelea na maandalizi ya mchezo wetu unaofuata.”
“Nimekamilisha mipango iliyonipeleka nyumbani Brazil, sasa ni muda wa kurudi kazini na kuendelea na timu pale nilipoishia ili kufikia malengo tulioyakusudia kuyafanya ndani ya timu.” amesema Robertinho
Simba SC baada ya mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya Singida Big Stars, itacheza mchezo wa Kimataifa wa Kirafiki dhidi ya Mabingwa wa Sudan Al Hilal ‘Omdurman’, kabla ya kusafiri kuelekea Guinea tayari kwa mchezo wa kwanza Hatua ya Makundi Ligi ya Mabingwa Barani Afrika dhidi ya Horoya AC.
Kwa sasa Wekundu hao wa Msimbazi wanashika nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara wakiwa na alama 50, wakitanguliwa na Watani zao wa Jadi Young Africans wenye alama 56.