Kikosi cha Azam FC leo Jumanne (Januari 31) kitapapatuana na Mabingwa wa Soka nchini Sudan Al Hilal ‘Omdurman’ walioweka kambi jijini Dar es salaam tangu juma lililopita.

Mchezo huo utakaoanza saa moja usiku, utakua wa pili kwa Al Hilal ‘Omdurman’ ambayo inajiandaa na Mshike Mshike wa Ligi ya Mabingwa Barani Afrika, ambapo itacheza dhidi ya Mabingwa wa Afrika Kusini Mamelodi Sundowns Februari 12.

Afisa Habari wa Azam FC Hasheem Ibwe amesema kikosi chao kipo tayari kwa mchezo huo wa Kimataifa wa Kirafiki na watautumia kuongeza uzoefu wa kikosi chao, kilichotinga hatua ya 16 Bora Kombe la Shirikisho Tanzania Bara ‘ASFC’.

“Wachezaji wapo tayari na maandalizi ambayo tumeyafanya yapo sawa, tunaamini kwamba tutapata matokeo chanya kwenye mchezo huu.”

“Mashabiki wajitokeze kwa wingi kwa ajili ya mchezo wetu muhimu ambao tutautumia kuongeza uzoefu.” amesema Ibwe

Al Hilal ‘Omdurman’ itakamilisha kambi yake jijini Dar es salaam kwa kucheza dhidi ya Simba SC Jumapili (Februari 05), Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam.

Taa za Mkwakwani kuwashwa
Robertinho: Ninarudi kuendelea na kazi