Kocha Mkuu wa Simba SC Roberto Olivieira ‘Robertinho’ amesema kikosi chake kinapaswa kupambana vilivyo nchini Uganda dhidi ya Vipers SC, ili kufufua matumaini ya kufuzu Hatua ya Robo Fainali.
Simba SC imepoteza michezo miwili ya Kundi C dhidi ya Horoya AC (Guinea) na Raja Casablanca (Morocco), hali inayoifanya kuburuza mkia wa kundi hilo.
Kocha Robertinho amesema kulingana na uhalisia wa msimamo wa Kundi C, kikosi chake kitapaswa kucheza kufa na kupona katika mchezo wa mzunguuko wa tatu, mwishoni mwa juma hili.
Amesema anaamini Wachezaji wake bado wana uwezo wa kucheza kwa kujituma na kupata matokeo mazuri katika Uwanja wa ugenini, hivyo kazi iliyobaki ni kufanya maandalizi kabambe na kucheza kwa malengo watakapoikuwa Uganda.
“Kulingana na hali yetu ilivyo kwenye kundi, tunahitaji nasi kwenda pale Uganda kushinda dhidi ya Vipers, Kama tukifanikiwa kupata ushindi na Vipers SC malengo yetu ya kufuzu hatua ya robo fainali yatakuwa kwenye hali nzuri”
“Wachezaji wangu wana uwezo wa kupambana na hawajakata tamaa, katika soka lolote linaweza kutokea, lakini ukweli ni kwamba, tunahitaji kushinda mchezo ujao ili kufufua matumaini yetu ya kusonga mbele.” amesema Robertinho
Simba SC kesho Jumanne (Februari 21) itacheza mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Azam FC, kisha itaelekea nchini Uganda, kwa mchezo wa Ligi ya Mabingwa Barani Afrika utakaopigwa Jumamosi (Januari 25).