Meneja wa Chelsea, Frank Lampard amemkingia kifua mchezaji wake Ross Barkley, ambaye usiku wa kuamkia leo alijitia lawamani, kwa kukosa mkwaju wa penati katika mchezo wa mzunguuko wa kwanza hatua ya makundi ya michuano ya ligi ya mabingwa barani Ulaya.
Lampard alichukua jukumu la kumtetea Barkley, akiwa katika mkutano na waandishi wa habari, baada ya mchezo huo kumalizika katika uwanja wa Stamford Bridge, huku wenyeji Chelsea wakikubali kulala kwa bao moja kwa sifuri dhidi ya Valencia ya Hispania.
Endapo Barkley angepata mkwaju wa penati, angeifanya timu yake kuambulia alama moja katika uwanja wa nyumbani, lakini ilikua tofauti na kuwaacha wageni wakiondoka jijini London na alama zote tatu.
Lawama nyingi zimeelekezwa kwa Barkley kwa kung’ang’ania kupiga penati hiyo huku akiwa sio chaguo la kwanza wala la pili la Chelsea katika upigaji wa penati, lakini Lampard ameamua kusimama na nyota wake na kudai kuwa hakuna tatizo.
“Ross ni mpigaji wa penati. Amefunga katika michezo kadhaa ya maandalizi ya msimu na leo (jana) ilikuwa apige wakati alipoingia na akakosa. Sijui majadiliano yalikuaje.
“Jorginho na Willian walikuwa ni wapigaji penati ndani ya uwanja na Barkley alipoingia naye akawa mpigaji penati na akakosa,” alisema Lampard.
Hata hivyo, meneja huyo amedai kuwa walikuwa na nafasi ya kupata ushindi kwenye mchezo huo pasipo kutegemea penati, lakini walishindwa kutumia vizuri nafasi walizopata.
“Tulipaswa kushinda au hata kutoka sare. Tulitengeneza nafasi za kutosha na pia tulipata penati na tulijikuta tukiruhusu bao kwa shuti lao moja tu lililolenga lango,” alisisitiza Lampard.
Bao pekee na la ushindi wa Valencia lilifungwa na Rodrigo Moreno, dakika ya 74, huku Chelsea wakikosa mkwaju wa penati katika dakika ya 87.
Mchezo mwingine wa kundi H ulishuhudia kikosi cha Ajax Amsterdam ya Uholanzi ikiishambulia Lille ya Ufaransa kwa kuifunga mabao matatu kwa sifuri.