Mwenyekiti wa Chama cha Marubani Tanzania, Kapten Aziz Abdallah amesema haamini kama Ndege ya Precision Air iliyopata ajali Mjini Bukoba Mkoani Kagera, ilikuwa haina mafuta ya kutosha na kusababisha ajali hiyo.
Akizungumza na Azam TV jijini Dar es Salaam, Kapteni Aziz amesema ni kosa kubwa kwa Ndege yoyote Duniani kupata ajali kwasababu ya kuishiwa mafuta kwani uratibu wa usafiri wa anga huzingatia umbali na tahadhari, na endapo itatokea dharula ya hali ya hewa, hitilafu au ajali katika kiwanja cha ndege kusudiwa, Rubani hatatakiwa kutua kiwanjani hapo.
Amesema, inapotokea hali ya dharula kama iliyokuwa katika mazingira ya Ndege hiyo aina ya ATR, humlazimu Rubani kwenda kutua katika uwanja mwingine na hivyo kuwa na akiba ya mafuta ya kuwezesha kufika uwanja husika na uwezo wa kuzunguka kwa takribani dakika 30 hadi 45 za ziada.
“Alikuwa na mafuta ya kutosha tangu anatoka Dar es Salaam, tumefundishwa kwamba hali ya hewa ikiwa mbaya au kuna ajali katika kile kiwanja huwezi kutua hivyo una dakika fulani ambazo unatakiwa uwepo pale, baada ya zile dakika lazima uondoke kwenda kutua sehemu ambayo uliweka kwenye ripoti yako kwamba ni kituo cha pili.”
Amesema, huenda Marubani hao mara bada ya kujadiliana walizunguka na kupitiliza dakika sahihi za kuendelea kuwa mahala pale, na hivyo kuishiwa mafuta ya kuwafikisha kituo cha pili cha kutua kwa dharula, hali iliyopelekea Ndege hiyo kupata ajali.
Kapteni Aziz ametoa ufafanuzi huo, baada ya ripoti ya pili ya uchunguzi wa ajali ya ndege ya Precision Air, iliyotokea Novemba 6, 2022 na kusababisha vifo vya watu 19 na majeruhi 24 kubaini mambo nane ikiwemo Marubani kutotilia maanani ishara za tahadhari zilizotolewa.
Wakati huo huo, Mkurugenzi Msaidizi, Sehemu ya Uchunguzi wa Ajali za Ndege, Redemptus Bugomola jana (Jumanne Machi 22, 2023), alisema katika ripoti ya kwanza walifika eneo la tukio na kuona jinsi ndege ilivyoumia, huku ripoti ya pili ikitoa ufafanuzi zaidi kwa kuangalia vinasa sauti na kupata mambo nane kama ifuatavyo-:
- Ndege ilikuwa imeandikishwa kihalali
- Marubani wa ndege hiyo hawakuwa na tatizo la kiafya
- Hali ya hewa katika uwanja wa ndege wa Bukoba haikuwa nzuri
- Hali mbaya ya hewa iliathiri marubani kutekeleza jukumu lao
- Marubani hawakutilia maanani ishara za tahadhari zilizotolewa
- Ndege iligonga kwanza bawa lake la kushoto wakati ikianguka
- Pia ilianguka kwa kasi na kugonga sehemu ya mbele kwenye kina cha maji ya ziwa
- Vifaa vyote vya kuongezea ndege vilikuwa vinafanya kazi kwa kuzingatia matakwa ya rubani
Ripoti ya awali ya ajali hiyo, ilitolewa Novemba 23, 2022 ambapo ilichambua mambo mbalimbali ya kitaalamu yalitokea wakati wa ajali hiyo.