Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), limesema limepokea kwa masikitiko vifo vya watu 19 waliokufa katika ajali ya ndege ya shirika la Ndege la Precision siku ya Jumapili Novemba 6, 2022, huku ikipendekeza wavuvi wote kuandaliwa kuwa Jeshi la Akiba la Uokozi kama ilivyo kwa Mgambo kwenye Jeshi la Nchi Kavu.

Taarifa hiyo iliyosainiwa na Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Deodatus Balile, imeeleza kuwa inatoa pole kwa familia zilizopoteza wapendwa wao, pia tunawaombea wote walioumia wapone haraka. Kadhalika, tunatoa pole kwa Kampuni ya Precision na Watanzania kwa ujumla kutokana na janga hili.

Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Deodatus Balile.

Taarifa hiyo imezidi kueleza kuwa, “Wakati huo huo, tukirejea matukio ya ajali yakiwamo hii ya ndege ya Precision, meli ya MV Bukoba, MV Spice Islander na nyingine zilizotokea majini, kimsingi zimepoteza maisha ya watu wengi kwa sababu ya uzembe na ukosefu wa vifaa vya uokoaji.”

Aidha, TEF imesema inatambua na kupongeza kazi kubwa ya uokoaji iliyofanywa na wavuvi wadogo katika ajali ya Precision na kdai kuwa hiyo si mara ya kwanza kwa wavuvi kufanya kazi ya kishujaa ya uokoaji kama hii kwani walifanya hivyo wakati wa MV Bukoba, MV Spice Islander na katika ajali nyingine za majini.

Ndege ya Precision Air iliyopata ajali Mkoani Kagera.

Kutokana na kazi ya uokoaji inayofanywa na wavuvi, TEF imesema inapendekeza wavuvi wote kuandaliwa kuwa Jeshi la Akiba la Uokozi kama ilivyo kwa Mgambo kwenye Jeshi la Nchi Kavu.

Aidha, imesema “Wakati tukiendelea na maombolezo, tunaisihi Serikali ifanye uwekezaji mkubwa katika mafunzo na vifaa vya uokoaji zikiwamo helikopta kwani hakuna mwenye uhakika kuwa ajali ya Precision majini ndiyo itakuwa ya mwisho.”

Mwijage ataka uchunguzi usafirishaji Mahabusu
Wawili wa familia moja wafariki katika ajali