Rais wa Kenya, William Ruto, amesema ataunda tume maalumu kuchunguza Makanisa na kutoa mapendekezo ya nini cha kufanyika ili kuepusha madhara kama yaliyotokea siku chache baada ya viongozi wa kidini kukamatwa kwa tuhuma za kutoa mahubiri potofu na kuhusishwa na mauaji ya waumini wao.
Ruto, ametoa kauli hiyo wakati ambapo Polisi ikiendelea kumshikilia Mhubiri tata Paul Mackenzie, ambaye katika eneo la shamba lake la Shakahola, miili ya watu zaidi ya 100 ilipatikana katika makaburi 23 wakiwa wamezikwa baada ya kufariki kwa mfungo tata wa kutokula hadi kufa ili waonane na MUNGU.
Kwa nyakati mbili tofauti, mwaka 2017 na baadaye 2018 kiongozi huyo wa kidini ambaye anashikiliwa na maofisa wa Polisi alikamatwa kwa kuhimiza watoto wasiende shule kwani alidai elimu haitambuliki katika Biblia, huku Maofisa wa upelelezi wakieleza kuwa wengi wa waliofariki ni watoto na wanawake.
Mwishoni wa wiki iliyopita hhubiri Ezekiel Odero wa kanisa la New Life Prayer Centre and Church, kupitia mawakili wake, amekiri kuwa watu 15 wamekufa wakati wakitafuta ushauri, katika kipindi cha miezi kumi na tatu, tangu kanisa hilo lilipoanzishwa ambapo kupitia mawakili wake Cliff Ombeta, Danstan Omari na Shadrack Wamboi, Odero alisema waliofariki, walienda kutafuta msaada wa kiroho wakiwa katika hali mbaya.