Rais wa Kenya, William Ruto amewashutumu wafanyakazi wa Mamlaka ya Mapato nchini humo KRA, kwa ukusanyaji wa mapato ya Serikali uliogubikwa na rushwa ukihusishwa na ushirikiano na wakwepa kodi, huku juhudi chanya zikiathiriwa na watendaji wasio waaminifu..
Ruto, ambaye alichaguliwa rais mwezi Agosti mwaka jana kwa ahadi ya kuwasaidia maskini, amekuwa akipitia changamoto nyingi katika miezi ya mwanzo ya utawala wake, kutokana na kuongezeka kwa ulipaji wa madeni ya serikali, upungufu wa ukusanyaji wa mapato na kupanda kwa bei za bidhaa.
Aidha, Watumishi wa umma pia wamekuwa wakilalamikia kuchelewa kulipwa mishahara yao katika miezi ya hivi karibuni, wakati mamlaka za serikali za mitaa zikitishia kufunga shughuli zao na kupinga uchelewesho wa kupatiwa pesa za malipo kutoka Serikalini.
Inaarifiwa kuwa, vitendo vya udanganyifu, kupokea rushwa na ufisadi umetawala shughuli za Mamlaka ya Mapato Kenya – KRA, kauli ambayo imetolewa na Rais Ruto wakati akiongea na wasimamizi wa mamlaka hiyo na wajumbe wa bodi.