Rais wa Kenya, William Ruto anatarajiwa kuanza ziara ya siku mbili nchini Tanzania Oktoba 09, ikiwa ni ziara yake ya kwanza katika nchi za Afrika Mashariki tangu alipoapishwa Septemba 13, kuwa Rais wa tano wa nchi hiyo.

Ziara ya kiongozi huyo nchini Tanzania inaashiria kuwa mahusiano yanayoendelea kujengwa na Rais Samia Suluhu Hassan yanafanya kazi katika kushirikiana kuleta maendeleo ya kijamii na kiuchumi kwa wananchi wao na Afrika Mashariki kwa ujumla.

Kwa kuifanya Tanzania kuwa nchi ya kwanza kutembelea katika Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) yenye nchi sita, inatoa ishara kwamba uhusiano wa Tanzania na Kenya unazidi kuimarika.

Alipokutana na Rais Samia jijini Nairobi, Kenya saa chache kabla ya kuapishwa, Ruto aliandika kwenye ukurasa wake wa Twitter akisema Serikali yake itashirikiana na Tanzania katika biashara, kilimo, usalama na maeneo mengine.

Rais Samia Suluhu Hassan na Rais William Ruto

“Tutapanua ushirikiano wetu na Tanzania katika biashara, kilimo, usalama miongoni mwa maeneo mengine yenye maslahi, mbali na kufanya kazi pamoja kwa nia ya kuijenga Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa manufaa yetu sote,” aliandika Ruto.

Rais Samia naye alipopata nafasi ya kuzungumza kwenye hafla ya kuapishwa kwa Ruto, aliwapongeza Wakenya kwa kuonyesha ukomavu kwenye uchaguzi uliofanyika Agosti 9 na kuwahakikishia Tanzania itaendelea kushirikiana na Kenya kuleta maendeleo.

Kenyatta kakwepa jukumu la amani Ethiopia?
Habari Kuu kwenye magazeti ya leo Octoba 08, 2022