Idara ya Habari na Mawasilino ya Klabu ya Ruvu Shooting, imetamba kikosi chao kitarejea Ligi Kuu Tanzania Bara msimu wa 2024/25, kutokana na mipango waliojiwekea watakapoanza kupambana katika Ligi ya Championship msimu ujao 2023/24.
Ruvu Shooting imeshuka daraja msimu wa 2022/23, huku ikiburuza mkia wa msimamo wa Ligi Kuu Tanzana Bara ikiwa na alama 20 kufuatia michezo 30 waliyocheza, lakini inaamini itakuwa na kila sababu ya kushiriki katika Ligi ya Championship kwa msimu mmoja pekee na kurejea ilipotoka.
Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasilino ya Rubu Shooting Masau Bwire amesema hawatarajii kucheza Championship zaidi ya msimu mmoja kwani wamejipanga kuhakikisha wanarudi ligi kuu.
Masau amesema watafanya maboresho ya kikosi chao muda wowote watakapotambua kuwa sehemu fulani kwenye kikosi kuna udhaifu.
“Hatuwezi kuwa tunafukuza makocha kila tunapofanya vibaya kwenye ligi badala yake huwa tunafanya tathimini kujua tatizo liko wapi kisha tunatafuta namna ya kulifanyia marekebisho, wachezaji tulio nao wanajua hapa tulipo Ruvu pakoje pia wanajua kuwa nini wanatakiwa kufanya.
“Tukiwa tunacheza ligi ya Championship, pale ambapo tutaona hapako sawa tutafanyia marekebisho na pale ambapo tutaona pako imara basi tutafanya vizuri na hatutegemei kucheza Championship kwa msimu zaidi ya mmoja,” amesema Masau.
Timu nyingine itakayoshiriki Ligi ya Championship ikitokea Ligi Kuu ni Polisi Tanzania ambayo ilimaliza katikanafasi ya 16 ikiwa na alama 25 baada ya kucheza michezo 30.