Serikali ya nchi ya Rwanda, imeishutumu Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo – DRC kwa kuyapuuza makubaliano yanayolenga kuleta amani katika eneo la mashariki la nchi hiyo linalokabiliwa na mgogoro.
Rwanda, imetoa shutuma hizo wakati mvutano kati yake na jirani yake ukiongezeka huku ikisema vitisho hivyo vimekuwa vikiongezeka na kuituhumu DRC kuwa inataka kujiondoa kwenye makubaliano yaliyofikiwa mjini Luanda nchini Angola na Nairobi.
Taarifa hiyo, pia imeilaumu Kongo kwamba inajaribu kuhujumu makubaliano ya kikanda na hatua hiyo inaweza kuonekana kuwa ya makusudi ya kuendeleza mgogoro na ukosefu wa usalama.
Januari 18, 2022 Waziri wa mambo ya nje wa DRC, Christophe Lutundula alilituhumu kundi la M23 na Serikali ya Rwanda kuwa kwa mara nyingine limeshindwa kutimiza ahadi zao, na kuapa kuwa Kongo itatumia kila njia kuhakikisha inalinda usalama wa eneo lake la mashariki.