Hatimaye Kocha Juma Mwambusi amemaliza utata hadharani na kukiri kuachana na Ihefu FC kwa makubaliano maalumu, huku mabosi wake wakibaki na kigugumizi.

Baada ya kutoonekana katika Benchi la Klabu hiyo ya Mkoani Mbeya wakati wa mchezo dhidi ya Young Africans, mashabiki wengi wamekuwa na sitafahamu baina ya Mwambusi na Ihefu FC wakijiuliza kinachoendelea baada ya kumtangaza kwa muda mfupi kisha kupotea kikosini kimyakimya.

“Sitaki iongezwe au kupunguzwa, ibaki kwamba nimeachana nao lakini kwa makubaliano maalumu, ishu ya kurudi au kutorudi achana nayo,” amesema kocha Mwambusi.

Hata hivyo siku mbili zilizopita Kocha Mwambusi alidai amejiweka kando kwenye kikosi hicho kwa ajili ya kushughulikia kwanza matatizo yaliyojitokeza ya kifamilia.

“Nimepumzika kidogo, nina majukumu mengine zaidi ya kuifundisha timu ya Ihefu, kwa muda huu sipo kwenye timu, kwa sasa ipo chini ya Zuberi Katwila ambaye yeye nimemkuta pale, nadhani kwa sasa wanaendelea vizuri kwenye mambo yao ya usajili kwa sababu mipango hiyo ilikuwa inaendelea.”

“Kuna mambo mengine yameingia kati hapa kwa hiyo nimeona kwanza niyashughulikie, akili yangu kwanza iwe kwenye hili jambo la kifamilia kwanza, nadhani baada ya kuweka sawa sawa nitakuwa na neno la kuzungumza kwa muda huu kwa kweli hakuna nitakachoelezea,” alisema Mwambusi.

Alikiri kuwa ni kweli hakuwepo kwenye kikosi tangu Januari 3 ambapo ilicheza mechi ya Ligi Kuu dhidi ya KMC na kushinda bao 1-0, huku akiongeza kuwa hana tatizo lolote lililomfanya aondoke na pia hakuna anachowadai.

“Mimi na Ihefu hakuna tatizo lolote, ndiyo maana hata wao wameruhusu nikashugulikie hayo matatizo kwa sababu wameona ni ya umuhimu vile vile, na hakuna ninachowadai,” aliongeza kocha huyo aliyetua kwenye klabu hiyo Septemba mwaka jana.

Wajawazito 210 wapoteza maisha kanda ya Magharibi
Rwanda yaituhumu DRC kwa kukiuka makubaliano