Wagonga nyundo wa jijini London West Ham United wamekamilisha usajili wa beki wa kulia Ryan Fredericks, akitokea kwenye klabu ya Fulham ambayo msimu wa 2018/19, itashiriki ligi kuu ya England baadaya kupanda daraja mwishoni mwa mwezi uliopita.
Fredericks anakua mchezaji wa kwanza kusajiliwa klabuni hapo, tangu uongozi wa West Ham Utd ulipomtangaza Manuel Pellegrini kuwa mkuu wa benchi la ufundi.
Meneja wa West Ham Utd Pellegrini aliyeajiriwa klabuni hapo baada ya kuondoka kwa David Moyes mwezi uliopita amesema, mchezaji huyo ni sehemu ya wachezaji aliowadhamiria kuwasajili katika kipindi hiki cha kuelekea msimu mpya wa ligi ya England.
‘Kusajiliwa kwa Ryan kumekamilisha sehemu ya malengo yangu, ninatarajiwa wakati wowote mchezaji mwingine atajiunga nasi, kwa ajili ya mapambano ya msimu ujao wa ligi, ambao ninatarajia utakua na ushindani mkubwa.
‘Ryan ni mchezaji mwenye uzoefu, ninaamini suala hilo litaleta changamoto mpya kwenye kikosi cha West Ham Utd.
Beki huyo mwenye umri wa miaka 25, kabla ya kukamilisha taratibu za kujiunga na West Ham Utd, alikua akiwaniwa na klabu za Crystal Palace na Newcastle Utd zinazoshiriki ligi kuu ya England.
Baada ya kuwa sehemu ya kikosi kilichokamilisha mpango wa kuipandisha daraja Fulham na kurejea ligi kuu baada ya miaka kadhaa, Ryan aligoma kusaini mkataba mpya na uongozi wa klabu hiyo ya jijini London, kwa shinikizo la kutaka kundoka na kwenda sehemu nyingine kusaka changamoto mpya za soka lake.