Watu saba wa familia moja wamefariki dunia usiku wa kuamkia leo (Mei 26, 2023), mashariki mwa nchi ya Uganda baada ya kutokea kwa maporomoko ya tope, yaliyotokana na mvua kubwa iliyonyesha wilaya ya Bulambuli.
Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo, Mkuu wa wilaya ya Bulambuli, Stanley Bayola amesema mvua hiyo iliyoambatana na upepo mkali ilinyesha kwa muda wa saa saba na kusababisha uharibifu mkubwa kwa makazi na mashamba ya watu wa eneo hilo.
Amesema, juhudi za kufukua maiti za wahanga na pia kuwanusuru baadhi ya watu waliokwama katika vifusi zinaendelea kwa sasa na inahofiwa kuwa idadi ya waliopoteza maisha inaweza kuongezeka kutokana na mazingira magumu ya kuwafikia watu wa familia kadhaa.
Hata hivyo, matukio ya maporokomo ya ardhi na tope hutokea mara kwa mara katika eneo hilo na watu hushauriwa kuchukua tahadhari katika msimu wa mvua lakini wengi wengi inawawia vigumu kuyahama makazi yao ya muda mrefu.