Mshambuliaji wa Mbeya City Sixtus Sabilo amekiri mambo yamekuwa magumu katika Michezo inayoihusu Klabu yao, baada ya kupoteza mchezo wa pili mfululizo wakiwa Dar es salaam.
Mbeya City ilipoteza dhidi ya Simba SC kwa kufungwa 3-2, siku ya Jumatano (Januari 18), huku wakitangulia kufungwa na Azam FC 6-1 (Desemba 30-2022).
Sabilo amesema licha ya kuwa na maandalizi mazuri, bado wanaendelea kusota katika matokeo mabaya, ambayo kila mmoja klabuni hapo hapendezwi na kinachowakuta.
Amesema hatua hiyo haijawakatisha tamaa, kwani watapambana zaidi ili kuirudisha Mbeya City katika kiwango kizuri, na kupata matokeo kwenye michezo iliyosalia msimu huu.
“Tunajiandaa vizuri na tumekuwa bora kwenye kiwanja cha mazoezi, ugumu unakuja baada ya dakika 90 kumalizika, tunajikuta tunamaliza mchezo kwa kipigo,”
Matokeo hayo hayajatukatisha tamaa, tunaendelea kupambana hadi mwisho kwa sababu lengo letu kuu ni kuhakikisha tunamaliza tano bora, kama tulivyoanza msimu huu tulikuwa katika nafasi nzuri. amesema mshambuliaji huyo aliyefunga mabao saba hadi sasa
Mbeya City ambayo imeshacheza michezo 20 ya Ligi Kuu Tanzania bara, inashika nafasi ya 10 katika msimamo, ikiwa na alama 21.