Kiungo kutoka nchini Mali Sadio Kanoute hatokuwa sehemu ya kikosi cha Simba SC kitakachoikabili Tanzania Prisons kesho Jumatano (Septemba 14).
Simba SC itakua Mgeni wa Tanzania Prisons, kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine Jijini Mbeya kuanzia saa kumi jioni.
Kabla ya kuanza safari ya kuelekea Mbeya leo Jumanne (Septemba 13) majira ya jioni, Kocha Mkuu wa Muda wa Simba SC Juma Mgunda alithibitisha kukosekana kwa kiungo huyo, kufuatia kuwa na maumivu ya jino, pamoja na kutumia adhabu ya kadi tatu za njano.
Mgunda amesema wachezaji wengine ambao watakosekana kwenye mchezo wa kesho Jumatano ni Kiungo kutoka Nigeria Victor Akpan pamoja na Shomari Kapombe waliokuwa majeruhi, lakini wameshaanza mazoezi ya wenzao.
“Kanoute hatokuwa sehemu ya kikosi cha Simba SC kwenye mchezo wetu wa kesho, anasumbuliwa na maumivu ya jino, pia hata kama angekua na afya njema asingweza kucheza kwa sababu anatumikia adhabu ya kadi tatu z njano.”
“Akpan na Shomari wamerejea mazoezini lakini hawana utimamu wa mwili, nao hawatoweza kuwa sehemu ya kikosi kwenye mchezo wetu wa kesho.” amesema Mgunda
Kuhusu Beki kutoka nchini Kenya Joash Onyango, Kocha Mgunda amethibitisha kurejea kwake na yupo safarini kuelekea Mbeya kuikabili Tanzania Prisons.
Mgunda amesema Beki huyo alijiunga na wenzake baada ya kuwasili kutoka Malawi na jana Jumatatu (Septemba 12) alifanya mazoezi ya pamoja, hivyo huenda akamtumia jijini Mbeya.
“Joash Onyango yupo kwenye kikosi, tunasafiri naye, amejiunga na wenzake tangu katika mazoezi ya jana, yupo tayari kwa mchezo hivyo tuombe aendelee kuwa na hali njema.” amesema Mgunda.
Mara ya mwisho timu hizo zilikutana msimu uliopita katika Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine, Simba SC ilikubali kupoteza kwa 1-0, bao likifungwa na Benjamin Asukile.