Aliyekuwa Kaimu Mwenyekiti wa Yanga Samwel Lukumay na aliyekuwa mjumbe wa kamati ya utendaji, akishikilia nyadhifa za Mwenyekiti wa Kamati ya mashindano na Mwenyekiti wa Kamati ya usajili, Hussein Nyika, wamejiuzulu nafasi zao leo Machi 27, 2019.
Nyika na Lukumay wametangaza hilo, kwenye makao makuu ya klabu hiyo ambapo wamesema kuwa wamefanya hivyo ili kupisha uchaguzi utaowezesha klabu hiyo kupata viongozi wapya.
Aidha, viongozi hao ndio waliokuwa wamebaki kwenye uongozi wa Yanga ambao uliingia madarakani mwaka 2016 baada ya wengine kujizulu, hivyo sasa timu hiyo inabaki bila uongozi mpaka pale uchaguzi mkuu utakapofanyika.
”Ninajiuzulu nafasi zangu zote nikiwa kama Mjumbe wa kamati ya utendaji lakini pia Mwenyekiti wa kamati ya usajili na kamati ya mashindano na niombe msamaha kwa wale niliowakosea katika utekelezaji wangu wa majukumu,” amesema Nyika.
Kwa upande wake Lukumay amesema kuwa wameamua kufanya hivyo ili kutoa nafasi kwa uchaguzi mkuu kupata viongozi wote tofauti na awali ambavyo ilikuwa ni uchaguzi mdogo wa kuziba nafasi.
Hata hivyo, siku za hivi karibuni Baraza la wadhamini la Yanga liliweka wazi kuwa, badala ya kufanya uchaguzi mdogo wa kuziba nafasi zilizowazi ikiwemo ile ya Mwenyekiti, utafanyika uchaguzi mkuu kwaajili ya kupata viongozi.