Klabu ya Sahare All Stars ya Tanga imetamba itacheza Fainali ya Kombe La Shirikisho Tanzania Bara (ASFC), itakayofanyika kwenye Uwanja wa Nelson Mandela mkoani Rukwa, mwishoni mwa mwezi huu.
Tambo za Sahare All Stars zimekuja baada ya kutinga hatua ya Nusu Fainali ya ASFC kwa kuichapa Ndanda FC ya mkoani Mtwara kwa penati nne kwa tatu, juzi Jumatano jijini Tanga.
Timu hizo zilifikia hatua ya matuta baada ya kumaliza dakika 90 zikiambulia matokeo ya sare ya bao moja kwa moja.
Afisa Habari wa Sahare All Stars, Shali Stambuli, amesema ushindi wao ni kazi nzuri ya viongozi, mashabiki na wachezaji wa timu hiyo ambao waliungana na kuamua timu yao ifanye vizuri kwenye mchezo wa Robo Fainali.
“Uongozi ulijipanga kuhakikisha tunashinda mchezo wetu dhidi ya Ndanda FC, tunamshukuru Mungu mipango yetu ilitimia na sasa tunajipanga kwa mchezo wa Nusu Fainali dhidi ya Namungo FC.”
“Tuna matarajio makubwa ya kuendelea kufanya vizuri kwenye mchezo wetu dhidi ya Namungo FC na kutinga hatua ya fainali, tunaamini tunaweza kufanya maajabu yatakayo washangaza mashabiki wa soka nchini.” Amesema Stambuli.
Klabu ya Sahare All Stars imeweka rekodi ya kuwa timu ya kwanza ya Daraja la Kwanza Tanzania Bara kufika hatua hiyo ya nusu fainali kwenye michuano hiyo.
Mchezo wa Sahare All Stars dhidi ya Namungo FC umepangwa kuchezwa Julai 11 uwanja wa CCM Mkwakwani jijini Tanga.
Mshindi wa mpambano huo atacheza fainali na mshindi kati ya Simba SC dhidi ya Young Africans watakaokutana Uwanja wa Taifa, Dar es salaam Julai 12.