Klabu ya Young Africans imetoa ufafanuzi kuhusu mchezaji Bernard Morrison, alieibua sakata la kutokua na mkataba wa miaka miwili na klabu hiyo, na badala yake anautambua mkataba wa miezi sita aliousaini wakati akiwasili nchini mapema mwaka huu.
Morrison ameibua sakata hilo baada ya kuhojiwa Global TV Jana Jumanne Dar es salaam, ambapo alisema mkataba wake wa miezi sita utafikia kikomo Julai 14.
Kufuatia taarifa hiyo ya Morrison, Uongozi wa Young Africans umetoa ufafanuzi kupitia taarifa rasmi iliyosainiwa na Kaimu Katibu Mkuu Simon Patrick inayoeleza kuwa, waliingia mkataba na mchezaji huyo Tarehe 15/01/2020 kwa ajili ya kuitumikia klabu hadi tarehe 14/7/2020, kwa kuwa na makubaliano endapo klabu itaridhishwa na kiwango chake mkataba utaongezwa.
Taarifa hiyo ya Young Africans imendelea kutoa ufafanuzi kwa kueleza, baada ya kuridhishwa na kiwango cha Morrison, tarehe 20/3/2020 klabu kwa maslahi binafsi ya mchezaji huyo waliingia makubaliano na kuongeza mkataba mpaka tarehe 14/7/2022.