Mkuu wa Kitengo cha Maudhui wa Simba SC, Ally Shatry amesema kiungo Mshambuliaji kutoka nchini Senegal Pape Ousmane Sakho yupo chini ya uangalizi maalum wa madaktari kufuatia majeraha aliyoyapata katika mchezo wao uliopita dhidi ya Dodoma Jiji FC.

Katika mchezo huo, Simba walilazimika kufanya mabadiliko matatu ya lazima kutokana na majeruhi ambapo alianza kutoka Pape Ousmane Sakho dakika ya 12 ya mchezo na nafasi yake kuchukuliwa na Rally Bwalya, dakika ya 41 Kennedy Juma alitoka na nafasi yake kuchukuliwa na Henock Inonga Baka, kabla ya dakika ya 63 Taddeo Lwanga kutoka na kuingia Duncan Nyoni.

Shatry amesema Sakho alipata majeraha makubwa, hivyo amewekea uangalizi mkubwa wa madaktari wa klabu ya Simba SC, ili kuangalia kama ataweza kurejea dimbani siku za karibuni.

Amesema wachezaji wengine waliokua majeruhi wamesharejea katika majukumu ya kujiandaa na mchezo wa mkondo wa kwanza wa Ligi ya Mabingwa Barani Afrika ambao utawakutanisha dhidi ya Jwaneng Galaxy mwishoni mwa juma lijalo.

“Kikosi kinaendelea na mazoezi ya kujiandaa na mchezo wetu ujao wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Jwaneng Galaxy ya Botswana ambao kwetu utakuwa mchezo wa kwanza katika michuano ya msimu huu.”

“Habari njema kwetu na kwa benchi la ufundi ni kuwa, tayari majeruhi wote wa kikosi wamepona na kuanza mazoezi, isipokuwa Pape Ousmane Sakho ambaye alipata majeraha katika mchezo wetu uliopita wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Dodoma Jiji, kwa sasa amewekwa chini ya uangalizi maalum wa madaktari ili kujua kama atakuwa tayari kwa ajili ya mchezo huo.” amesema Shatry

Simba SC itaanzia ugenini Bostwana kucheza mchezo wa mkondo wa kwanza wa Ligi ya Mabingwa Barani Afrika dhidi ya Jwaneng Galaxy Oktoba 17, huku mchezo wa mkondo wa pili ukipangwa kuchezwa Uwanja wa Benjamin mkapa, jijini Dar es salaam Tanzania Oktoba 22.

Taifa Stars kuifuata Benin leo
Jwaneng Galaxy waitumia salamu Simba SC