Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amewasilisha salamu za pole kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, kwa wananchi waliokumbwa na athari baada ya tembo kuvamia vijiji vyao na kusababisha maafa ikiwemo kifo.
Akiongea na wananchi katika kijiji cha Nditi Wilayani Nachingwea, Waziri Mkuu amesema amefika hapo kwa ziara ya kikazi na kukagua athari zilizosababishwa na uvamizi wa tembo katika mashamba ya wananchi kwenye kijiji cha Namapwiya.
“Rais wetu anawapa pole kutokana na athari hizo na hapa namuagiza Mkuu wa Wilaya kupitia kamati ya maafa ya wilaya ahakikishe wanaandaa utaratibu wa kupatikana chakula kwa wananchi wote ambao mashamba yao yameathiriwa na wanyamapori,” amesema Majaliwa.
Amesema, tatizo hilo pia limechangiwa na wafugaji waliovamia maeneo ya hifadhi kwa kuingiza mifugo na kusababisha wanyamapori kukimbia na kwenda kwenye makazi ya wananchi.
Hata hivyo, Waziri Mkuu amemwagiza Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki kukutana na wafugaji na kuwataka kutopeleka ng’ombe na mbuzi kwenye maeneo ya hifadhi ikiwemo Wananchi kutoingia na kuendesha shughuli za kilimo katika maeneo hapo.
Akiwa katika kijiji cha Namanja kilichopo kata ya Nditi, kabla ya kuzungumza na wananchi Waziri Mkuu Majaliwa alikwenda kuifariji familia ya marehemu Riziki Issa, ambaye aliuawa na tembo na kisha kuwapa pole na salam za Rais Samia.
Akizungumza kwa niaba ya familia hiyo, Mussa Nambole amesema wamefarijika kwa namna ambavyo viongozi mbalimbali wa Serikali walivyoshirikiana nao katika kipindi chote cha msiba huo na kuwaombea heri kwa Mwenye enzi Mungu.
Kwa upande wake Mbunge wa Nachingwea. Dkt. Amandus Chingwile ameishukuru Serikali kwa kuweka mikakati mbalimbali inayolenga kuzuia uvamizi wa wanyamapori kwenye makazi ya wananchi kitu ambacho kitasaidia kuondoa athari wa muingiliano wa wananchi na wanyama katika maeneo yao.