Serikali kupitia Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo inaendelea na uratibu wa maandalizi ya ujenzi wa Sanamu ya Mwl. Nyerere inayotarajiwa kusimikwa Jijini Addis Ababa Ethiopia katika Makao Makuu ya Umoja wa Afrika.
Hayo yamebainishwa na Waziri wa Utamaduni Sanaa na Michezo, Pindi Chana ambaye amesema hadi Aprili, 2023 hatua iliyofikiwa ni kuanza kwa ujenzi wa Sanamu halisi baada ya Mkandarasi, Kampuni ya EPITOME ARCHITECTS LIMITED ya Tanzania kukamilisha ujenzi wa sampuli kifani ya pili na kuridhiwa na Kamati ya Kitaifa kwa mujibu wa Sheria ya kuwaenzi Waasisi wa Taifa Na. 18 ya mwaka 2004 na Kanuni zake za mwaka 2005.
Chimbuko la Mradi huo ni mapendekezo ya Hayati Robert Mugabe la mwaka 2015 yaliyolenga kutambua mchango uliotukuka wa Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere katika ukombozi wa Bara la Afrika hasa Mataifa yaliyo Kusini mwa Bara hilo.
Mradi huo wenye thamani ya Dola za Marekani 205,942 unajengwa chini ya usimamizi wa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Sekretarieti ya SADC, Mameneja Mradi kwa kushirikiana na familia ya Mwalimu Nyerere na kwa mujibu wa Mkataba uliopo, inatarajiwa kukamilika Desemba, 2023.