Saudi Arabia imeandika historia kwa kuruhusu wanawake kuendesha magari kwa mara ya kwanza baada ya miaka mingi ya mapambano ya wanaharakati waliodai haki hiyo.
Nchi hiyo ilikuwa nchi pekee duniani iliyopiga marufuku wanawake kuendesha magari hivyo leseni za udereva zilitolewa kwa wanaume pekee.
Baadhi ya wanawake waliojaribu kuvunja sheria hiyo walikutana na mkono wa sheria kwa kufungwa jela au kutozwa kiwango kikubwa cha faini.
Viongozi mbalimbali duniani pamoja na wanaharakati wameipongeza hatua hiyo ambayo inaongeza tija katika mchakato wa kuwakomboa wanawake dhidi ya mfumo dume.
Rais wa Marekani, Donald Trump ni mmoja kati ya waliotoa maoni yake kwamba hiyo ni ‘hatua chanya’ kuelekea katika usawa wa kijinsia.
Mwanaharakati, Sahar Nassif ambaye alikuwa msitari wa mbele kudai haki hiyo kwa wanawake amesema kuwa amefurashishwa na uamuzi huo na kwamba atajinunulia gari la ndoto yake kuweka kumbukumbu ya furaha yake.
“Nimefurahi sana, nimeruka juu na kucheka mara kadhaa. Nitanunua gari jipya la ndoto yangu [kuweka kumbukumbu ya furaha yangu]. Litakuwa na rangi nyeusi na njano,” aliiambia BBC.
Balozi wa Saudi Arabia nchini Marekani, Prince Khaled bin Salman amethibitisha kuwa wanawake hawatakuwa na haja ya kupata kibali kutoka kwa waume zao kujiunga na mafunzo ya udereva na wakaweza kuendesha gari popote wanapopenda.