Rais wa Kenya, Dkt. William Ruto amewataka wafanyabiashara kulipa mikopo ya ‘Hasla Fund’ waliochukua ili kuanzisha biashara zao huku akisema kuna watu wanagoma kulipa kwa madai kuwa walimpigia kura kitu ambacho si sawa.
Akizungumza katika Kaunti ya Embu nchini humo, Dkt. Ruto aliapa kuhakikisha waliochukua mikopo hiyo ambayo inatozwa riba ya asilimia nane, inalipwa yote.
Alisema, “Hasla Fund si pesa za bure. Huo ni mkopo na ni pesa ambazo lazima zirudishwe kwa serikali, tulitaka Wakenya kufaulu kujipatia mkopo kwa njia rahisi kujinufaisha kibiashara na hawafai kuichukulia kama kwamba ni pesa za bwerere.
“Kuna watu wanasema walinipigia kura na hivyo wanastahili kubaki na pesa hizo, la, si hivyo, haikubaliki. Pesa zilizotolewa ni deni na lazima zilipwe, sasa nitazindua mkondo wa pili wa hazina hiyo wakati wa sikukuu ya Madaraka Dei ili Wakenya wanufaike zaidi,” ameongeza Ruto
Hata hivyo ameongeza kuwa, katika awamu ya pili wa mikopo hiyo , Wakenya watafanikiwa kujipatia kati ya Shilingi 20,000 hadi 200,000 bila dhamana yoyote, huku akiwataka Wakenya kuendelea kujikuza kibiashara kwa kutumia kwa uangalifu fedha hizo ili ziwapatie faida.