Uongozi wa Chuo Kikuu cha Dar es salaam, umewasimamisha masomo baadhi ya viongozi wa Serikali ya wanafunzi wa DARUSO, akiwemo Rais Hamis Musa kwa kukiuka taratibu na sheria za chuo hicho, ikiwa ni siku chache baada ya kuipa Bodi ya Mikopo saa 72 kusikiliza mahitaji yao.
Katikia Barua ambayo imesainiwa na Makamu Mkuu wa Chuo hicho Prof. William Anangisye imesema viongozi hao wamekiuka taratibu na sheria za Chuo hicho.
Sasa viongozi hao wanatarajiwa kufikishwa kwenye Kamati ya Nidhamu kwa ajili ya kusikiliza shauri lao.
Juzi DARUSO walitoa saa 72 kwa Bodi ya mikopo ya wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB), kuhakikisha inatoa mikopo kwa wanafunzi waliokosa, vinginevyo watakutana nje ya ofisi za bodi hiyo.
Waziri wa Elimu, Prof. Joyce Ndalichako alisema kwa mujibu wa taratibu, Uongozi wa DARUSO ulipaswa kuwasiliana na Mshauri wa Wanafunzi ambaye anachukua malalamiko yao na kuyapeleka kwa Makamu Mkuu wa chuo.
Profesa Ndalichako alisema tamko hilo limetolewa kinyume cha utaratibu wa kutoa malalamiko na ni utovu wa nidhamu wa kiwango cha juu ambacho hakiwezi kuvumilika, hivyo alitoa saa 24 kwa uongozi wa chuo UDSM kuwachukulia hatua viongozi wa DARUSO na apewe taarifa, jambo ambalo tayari limetekelezeka.