Mwanamke mmoja nchini Uingereza ameanguka nje ya dirisha la gari lililokuwa linaenda kasi baada ya kutoa kichwa nje na kuning’inia akijirekodi video ya Snapchat.
Kitengo cha Polisi kinachosimamia usalama barabarani nchini Uingereza, kimeandika kisa hicho kwenye akaunti yake ya Twitter, kikieleza kuwa alianguka katikati ya Barabara ya M25 katika jiji la London yenye magari mengi yanayoenda kasi katika.
“Kwa bahati nzuri mwanamke huyo hakupoteza maisha na hakupata majeraha makubwa,” imeeleza taarifa hiyo.
Kwa mujibu wa utafiti uliochapishwa kwenye Jarida la Family Medicine and Primary Care, watu 259 duniani kote walipoteza maisha wakati wa kujipiga picha za selfie kati ya mwaka 2011 na 2017.
Utafiti huo ulibaini kuwa vifo vingi zaidi viliripotiwa nchini India, ikifuatiwa na Urusi, Marekani na Pakistan.
Mwaka jana, watu wanne wa familia moja nchini India walipoteza maisha baada ya kutereza na kutumbukia kwenye bwawa lenye kina kirefu walipokuwa wakijaribu kujipiga selfie.
Ingawa kwa kawaida ungemuuliza Mtanzania angeweza kudhani waathirika wakubwa wa upigaji picha za selfie watakuwa wanawake, utafiti huu umeonesha kuwa wanaume ndio wahanga zaidi wa selfie za kifo.
Takribani asilimia 72 ya walioripotiwa kupoteza maisha wakijirekodi selfie au Snapchat ni wanaume. Kwa kigezo cha umri, ni asilimia 30 tu ya wenye umri chini ya miaka 18 ndio waliopoteza maisha katika mazingira hayo.