Promota wa masumbwi nchini Tanzania Suleyman Semunyu amekanusha tuhuma za kutomlipa Bondia kutoka DR Congo Keyembe Tshibangu ambaye kwa sasa yupo nchini akisubiri pambano lake dhidi ya Twaha Kiduku litakalounguruma kesho Ijumaa (April 09), kwenye ukumbi wa Ubongo Plaza jijini Dar es salaam.
Bondia Tshibangu alidai kutokulipwa sehemu ya fedha zake na Promota huyo ambaye alimuandalia pambano la kimataifa dhidi ya Hassan Mwakinyo lililounguruma mwaka 2020, kwenye Ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es salaam.
Semunyu amesema baada ya kusikia tuhuma hizo alifadhaika na kuona Tshibangu amemkosea heshima, kwani ukweli wote wa kulipwa fedha zake kabla ya kupanda ulingoni kupambana na Mwakinyo, alikua akufahamu kwa usaidizi wa meneja wake na balozi wa DR Congo nchini Tanzania.
“Nilishutushwa na taarifa alizozitoa Tshibangu, lakini ukweli ni kwamba alilipwa pesa zake zote kabla ya kupanda ulingoni kucheza dhidi ya Hassan Mwakinyo siku ile,”
“Meneja wake alihakiksha analipwa, pia walimshirikisha balozi wa DR Congo hapa nchini katika suala hilo la malipo, sasa anaposema hajalipwa inanishangaza sana.”
“Nilipanga kumfikisha kwenye vyombo vya sheria ili athibitisha hakulipwa ama amelipwa, lakini nimeona nitaharibu pambano ambalo limeandaliwa na mtanzania mwenzangu Promota Mopao, kesho ijumaa (April 09), ambapo Tshibangu atacheza dhidi ya mtanzania Twaha Kiduku.”
“Ninachomuomba Tshibangu aseme ukweli, kwa sababu kila kitu kiliwekwa wazi na viongozi wa kamisheni ya ngumi Tanzania walishuhudia hilo, kabla hajapambana na Mwakinyo, kwenye ukumbi wa Mlimani City.”
Katika hatua nyingine Semunyu akatumia nafasi ya kuzungumza na Dar24 Media ‘Taarifa Bila Mipaka’ kueleza namna alivyojipanga katika kuandaa mapambano ya ngumi baada ya Tanzania kumaliza msiba John Pombe Joseph Magufuli aliyefariki dunia Machi 17 na kuzikwa nyumbani kwake wilayani Chato mkoani Geita.
“Kwa sasa nimedhamiria kumuunga mkono Rais Samia Hassan Suluhu, ambaye ametutaka tuwape kipaumbele wanawake kwenye michezo, nimeandaa pambano la ngumi ambalo lifafanyika kwenye ukumbi wa Ubungo Plaza, kati ya Halima Vunja Bei dhidi ya Zulfa Macho” amesema Semunyu.
Semunyu ni mdau wa michezo wa ngumi za kulipwa kwa muda mrefu, huku akiwa sehemu ya walionesha kurejesha hadhi ya mchezo huo tangu ulipojijengea heshima wakati wa serikali ya awamu ya tano chini ya Hayati John Pombe Joseph Magufuli.