Kamisaa wa Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022, Anne Makinda amewapongeza Waandishi wa Habari kwa kuelimisha na kuhamasisha Umma wakati wa zoezi la Sensa ya Watu na Makazi Mwaka 2022, huku akiwataka kuendeleza kazi hiyo kwa kuandika Habari sahihi za matokeo ya Sensa yanayoendelea kutolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu -NBS.
Makinda ameyasema hayo mjini Njombe, wakati wa ufunguzi wa mafunzo kwa Waandishi wa Habari wa Mikoa ya Njombe na Ruvuma, ili waweze kuandika na kuripoti kwa ufasaha matokeo ya Sensa ya Watu na Makazi yanayoendelea kutolewa na Ofisi hiyo ya NBS.
Amesema, “wakati wa Sensa ya mwaka 2022 mlifanya kazi nzuri ya kuelimisha wananchi, sasa matokeo yanaendelea kutolewa, tunaamini kwamba mtatumia mafunzo haya kufanya kazi ya kutafsiri matokeo yanayotolewa ili wananchi wayatumie kufanya maamuzi.”
Hata hivyo, Makinda amesema Nchi yoyote Duniani ikitaka kuendelea lazima itumie takwimu sahihi na Tanzania inazalisha takwimu ambazo Waandishi wa Habari wanao wajibu wa kuwaelimisha wananchi ili wazitumie, ambapo mafunzo hayo ya siku mbili yakitarajiwa kumalizika hii leo Septemba 19, 2023.