Kamishna wa Sensa ya Watu na Makazi, Anne Makinda amesema zoezi la Sensa ya Watu na Makazi linaloendelea kufanyika nchini kote, limevuka lengo na kufikia zaidi ya asilimia 17 tofauti na makadirio ya awali yaliyowekwa ya kuandikisha watu kwa asilimia 15.
Makinda ameyasema hayo wakati akiongea na vyombo vya Habari, na kusema uandikishaji huo wa zaidi ya asilimia 17, umefikiwa licha ya changamoto mbalimbali zilizojitokeza za kuibwa kwa vitendea kazi, kama vishikwambi vya makarani na malalamiko ya baadhi ya wananchi juu ya kusubiri kwa muda mrefu huduma hiyo.
Amesema, “ushirikiano wa wananchi, makarani na vyombo vya ulinzi na usalama uliweza kufanikisha kukamata vitendea kazi vilivyoibiwa, huku sehemu kubwa ya raia wakisifia umahiri wa waratibu wa zoezi zima la Sensa kitaifa.”
Baadhi ya wananchi waliohojiwa na wanahabari, wamesema wengi wao walikuwa wakilisubiri zoezi hilo kwa umakini, na kwamba Makarani wengi waliweza kusimamia majukumu yao kwa umakini na kwa kuzingatia wakati.
Mmoja wa wananchi waliohesabiwa, Salehe Lezeli amesema, “Mambo yamebadilika na teknolojia imekuwa hivyo kilichotokea ni ugeni tu wa kimazingira umesababisha wengi wetu kutoelewa kwa haraka lakini kadri muda ulivyokuwa ukienda mambo yalikuwa ni safi na nikahesabiwa,”
Kamishna wa Sensa ya Watu na Makazi, Anne Makinda akitoa tathimini ya zoezi hilo amesema mambo yanaenda vizuri, kutokana na asilimia kubwa ya zilizopo nchini kurekodiwa katika kituo cha kuchakata sensa katika kituo kilichopo Makao Makuu ya Nchi Dodoma.
Zoezi la Sensa ya watu na makazi hii leo Agosti 26, 2022 limeingia katika siku yake ya nne, ambapo Watanzania wengi wanaendelea kuhesabiwa ili Serikali iweze kutambua idadi ya watu kwa ajili ya kupanga mipango itakayowezesha kusogeza huduma za kimaendeleo kwa Wananchi.