Mbunge wa Vunjo, Dkt Charles Kimei amesema deni la taifa ni himilivu na thamani ya shilingi ni nzuri ambapo Serikali inaweza kutumia kwenda kukopa fedha kwenye soko la dunia kwa riba ndogo ili kukamilisha miradi mikubwa nchini.
Amesema hayo bungeni Jijini Dodoma alipokuwa akichangia mjadala wa kupitisha mpango wa tatu wa maendeleo ya kitaifa kwa kipindi cha miaka mitano kuanzia 2021/22 – 2025/26.
Aidha ameipongeza Serikali kwa kuuweka uchumi wa nchi kwenye hali ya utulivu na nzuri katika kipindi cha ugonjwa wa Covid-19 na mfumuko wa bei uko chini.
“Tunaona hali ya deni la taifa ni himilivu na thamani ya shilingi yetu iko nzuri hiyo ni faida kubwa ambayo tunaweza kuitumia kufanya utafiti na kwenda kukopa kwa riba ya chini sana ya asilimia 5 au 6 kwa kukopa moja kwa moja ili tukamilishe ujenzi wa miradi mikubwa tunayoendelea nayo” amesema
“Hakuna sababu ya kuchelewesha wa utekelezaji wa ujenzi wa miradi mikubwa kama SGR na mradi wa umeme wa Mwalimu Nyerere wakati tunaweza kukopa na kukamilisha haraka na kuona matunda kwa miradi hiyo mikubwa ambayo ni chachu katika ukuaji wa taifa letu,”amesema Kimei
“ Tusizingatie kukopa ndani kwa sababu tunatakuwa tunaumiza sekta binafsi kwakuwa hawawezi kwenda kukopa nje kwasababu hawajulikani, Serikali inajulikana na kama tukihamasika kwenda kukopa nje na kuacha resources za ndani zikakopwa na watu binafsi kwanza riba zitakuwa chini,” amesema Kimei