Mbunge wa Vunjo, Dkt Charles Kimei amesema deni la taifa ni himilivu na thamani ya shilingi ni nzuri ambapo Serikali inaweza kutumia kwenda kukopa fedha kwenye soko la dunia kwa riba ndogo ili kukamilisha miradi mikubwa nchini.

Amesema hayo bungeni Jijini Dodoma  alipokuwa akichangia mjadala wa kupitisha mpango wa tatu wa maendeleo ya kitaifa kwa kipindi cha miaka mitano kuanzia 2021/22 – 2025/26.

Aidha ameipongeza Serikali kwa kuuweka uchumi wa nchi kwenye hali ya utulivu na nzuri  katika kipindi cha ugonjwa wa Covid-19 na mfumuko wa bei uko chini.

“Tunaona hali ya deni la taifa ni himilivu  na thamani ya shilingi yetu iko nzuri  hiyo ni faida kubwa ambayo tunaweza kuitumia kufanya utafiti na kwenda kukopa kwa riba ya chini sana  ya asilimia 5 au 6 kwa kukopa moja kwa moja ili tukamilishe ujenzi wa miradi mikubwa tunayoendelea nayo” amesema

 “Hakuna sababu ya kuchelewesha  wa utekelezaji wa ujenzi wa miradi mikubwa kama SGR na mradi wa umeme wa Mwalimu Nyerere wakati tunaweza kukopa na kukamilisha haraka na kuona matunda kwa miradi hiyo mikubwa ambayo ni chachu katika ukuaji wa taifa letu,”amesema Kimei

“ Tusizingatie kukopa ndani kwa sababu  tunatakuwa tunaumiza sekta binafsi kwakuwa hawawezi kwenda kukopa nje kwasababu  hawajulikani, Serikali inajulikana na kama tukihamasika kwenda kukopa nje na kuacha resources za ndani zikakopwa na watu  binafsi kwanza riba zitakuwa chini,” amesema Kimei 

Tarimba aishauri Serikali kuwatumia wawekezaji wa ndani
Viongozi SADC walaani uasi Msumbiji